International Journalist covering Africa with over 7 years of reporting. Current Board Chair of the Foreign Press Association, Africa.
Kiongozi wa Upinzani nchini Kenya Raila Odinga baada ya kukutana na kundi la wabunge wa chama chake Alhamisi ambapo ametangaza timu ya kufanya mazungumzo na serikali ya rais William Ruto, amesema kambi yake imeazimia kushinikiza ufanyikaji wa marekebisho
Tangu enzi za Ukoloni,Kenya imekuwa ikikumbwa na maadui watatu.Rais mwanzilishi wa taifa hilo la Afrika Mashariki, Hayati Jomo Kenyatta alitambua maadui wa tatu wa Kenya kuwa ukabila,ujinga na ugonjwa na kutangaza kukabiliana na maadui hao. Hadi wa leo nchi hiyo imekuwa ikikumbwa na ukabila ambao umekuwa ukikithiri katika taasisi kuu za nchi hiyo pamoja na asasi muhimu. Ripoti ya Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa nchini humo inaeleza kuwa nyadhifa kubwa za kazi muhimu katika mashirika ya kiserikali zimechukuliwa na makabila machache yenye ushawishi mkubwa kinyume na sheria inayodhibiti kuajiriwa kwa watu wa kabila moja katika idara kuu za serikali. Mwandishi wetu wa Nairobi,Kennedy Wandera, amezungumza na wakenya na kutuandalia taarifa ifuatayo ambayo imezua hisia kali nchini humo.
Shambulizi la leo lililotekelezwa na wanamgambo wa Alshabaab na kuwaua watu kumi na wawili katika hoteli ya Bishaaro katika mji wa Mandera nchini Kenya ni mfululizo wa mashambulizi na kundi hilo la kigaidi nchini humo tangia Kenya ipeleke majeshi yake katika nchi ya Somalia. Ni kutokana na hali hii ambapo Rais Uhuru Kenyatta leo amekatiza ziara yake rasmi katika nchi ya Angola kuhudhuria mkutano wa usalama ili kuomboleza na familia zilipatwa na msiba huo. Sasa naibu Rais wan chi hiyo ya Afrika Mashariki William Ruto atamwakilisha Rais katika mkutano huo. Lakini suala ambalo limekuwa likigonga vyombo vya habari na kushangaza wengi ni ushirikiano unaonekana kuwepo kati ya wenyeji na wanamgambo hao. Na je, hivi ni vita vinavyofanywa kimakusudi kwa misingi ya kisiasa baina ya wanasiasa wa ukanda huo? Mwandishi wetu wa Nairobi,Kennedy Wandera, ametuandalia taarifa ifuatayo.
Kutokana na tuhuma za utepetevu wa madaktari wa hospitali mbili jijini Nairobi nchini Kenya, hususan katika kifo cha Alex Madaga mwenye umri wa miaka 37 mwaka uliopita, anayeripotiwa kutopewa huduma ya dharura baada ya kugongwa na gari na kupata majeraha ya kichwani, darubini imeangaziwa vituo vya kiafya vinavyotoa huduma ya dharura nchini humo, baada ya kufahamika kuwa mgonjwa huyo alilazimika kushinda masaa kumi na nane ndani ya ambulensi. Lakini je,mgonjwa anayehitaji huduma ya dharura anastahili kupata huduma hiyo kwa njia gani? Na je,wakenya waliopoteza jamaa zao katika mazingira sampuli hiyo wanaelezaje? Mwandishi wetu wa Nairobi,Kennedy Wandera, ametuandalia makala ifuatayo.
Leo ulimwengu unapoadhimisha siku ya Ukimwi duniani, Kenya nayo imejiunga na mataifa hayo kutokomeza maambukizi ya virusi vya Ukimwi. Katika taifa hilo la Afrika Mashariki, takwimu za sasa zinaonesha kuwa idadi ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi imeongezeka kutoka milioni 1.4 mwaka wa 2009 hadi milioni 1.6.Lakini mara kwa mara juhudi za kutokomeza maambukizi haya zimekuwa zikielekezewa watu wazima na watoto, na kusahau vijana waliovunja ungo. Je, takwimu nchini humo zinaelezaje kuhusu maambukizi mapya kwa vijana? Mwandishi wetu wa Nairobi,Kennedy Wandera, ametuandalia taarifa ifuatayo.
Mafunzo ya itakadi kali yamekuwa yakienezwa na makundi haramu na ya kigaidi ili kuendeleza juhudi zake kuangamiza na kushinikiza Kenya kuondoa majeshi yake nchini Somalia. Lakini huku Kenya ikiwa imeimarisha jitihada zake kukabiliana vikali na makundi haya haramu, suala ambalo limekuwa likigonga vichwa vya habari ni jinsi makundi haya ya kigaidi yanavyojipenyeza nchini na kuwapa vijana hususan wa vyuo vikuu nchini humo mafunzo ya itikadi kali. Ni kutokana na hili ambapo viongozi wa vyuo vikuu nchini Kenya wanakongamana katika Chuo Kikuu cha Nairobi kutafuta mikakati ya kuwahimiza wenzao kutojihusisha na juhudi zozote zinazopania kukwamiza mustakabali wa nchi yao. Mwandishi wetu wa Nairobi,Kennedy Wandera, amehudhuria kongamano hilo na kutuandalia taarifa ifuatayo.
Huku mkutano wa tatu wa kikao cha tano cha Bunge la Afrika Mashariki uking’oa nanga leo jijini Nairobi nchini Kenya kwa majuma mawili yajayo, kinachosubiriwa katika kikao hiki ni kuidhinishwa na kupitishwa kwa mswada unaodhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki almaarufu Polythene Materials Control Bill. Japo udhibiti wa matumizi ya bidhaa za plastiki umekosa kutekelezwa nchini Kenya, zipo ishara kuwa kupitishwa kwa mswada huu kuwa sheria kutailazimisha Kenya kukumbatia maamuzi ya Bunge la Afrika Mashariki. Je, wanaharakati wa mazingiria wanaelezaje?
Katika kile kinachoonekana kama jitihada za kutimiza na kutekeleza ahadi zake kabla ya uchaguzi wa mwaka ujao, Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, imetangaza rasmi kuanza kuwapa wanafunzi wote wa shule za msingi za umma katika taifa hilo vipakatalishi kuanzia leo zoezi litakalotamatika kwa siku thelathini. Mara tu baada ya kuchaguliwa katika kura ya mwaka 2013, Rais Kenyatta aliahidi kuyafanya masomo kuwa kwenye mfumo wa kidigitali kwa kuwapa wanafunzi wote wa shule za umma nchini humo vipakatalishi hivyo. Mwandishi wetu wa Nairobi Kennedy Wandera, ametuandalia taarifa ifuatayo
Siku moja tu baada ya Shirika la Kimataifa la kupigania haki za Kibinadamu la Amnesty International kuishtumu Kenya kwa kuwashinikiza wakimbizi walioko kwenye kambi ya wakimbizi ya Dadaab kugura kambi hiyo, Kenya imeamua kuongeza makataa ya kufunga kambi hiyo hadi baada ya miezi sita. Taifa hilo la Afrika Mashariki linasema limeafikia uamuzi huo ili kuipa jamii ya kimataifa muda kuhakikisha wakimbizi hao wanaorejeshwa makwao wanapata makao yaliyo na usalama. Mwandishi wetu wa Nairobi,Kennedy Wandera, ametuandalia taarifa hiyo kwa kina.
Takriban miezi mitatu baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Kenya ya Maadili na Kupambana na Ufisadi Philip Kinisu kwa tuhuma za kuhusishwa kampuni ya familia yake katika sakata ya Shirika la Huduma kwa Jamii yaani NYS, Tume ya Huduma kwa Umma nchini humo hivi leo imeandaa kikao kuwahoji watu sita waliotuma maombi kuchukua wadhifa huo ulioachwa wazi. Lakini, Mbona tume hii imekuwa ikionekana dhaifu katika juhudi zake za kupambana na Ufisadi? Na Je, ni kipi hasa kinachofaa kutekelezwa kuimarisha tume hiyo ambayo imekuwa ikiyumbayumba kila mara? Mwandishi wetu wa Nairobi, Kennedy Wandera, ametuandalia taarifa ifuatayo